Share news tips with us here at Hivisasa

Katibu wa Serikali ya kaunti ya Mombasa Francis Thoya ameitaka Tume ya Kitaifa ya Ardhi kuwatengea kipande cha ardhi maskwota wanaodaiwa kuishi katika ardhi zisizokuwa zao.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, Thoya alisema kwamba iwapo utaratibu mwafaka utatumika wa kuwatengea maskwota hao sehemu ya kuishi, basi mgogoro baina yao na wamiliki wa ardhi itasitishwa.

Kulingana na Thoya, ardhi zinazozozaniwa katika kaunti hiyo zimechangiwa pakubwa na watu kunyakua ardhi na kufurusha wenyeji, huku akisema kwamba swala hilo litapata suluhu kwa ushirikiano.

“Tunaiomba tume ya kitaifa ya ardhi inayoongzwa na mwenyekiti wake Dkt Mohammed Swazuri kuwatengea maskwota wa Mombasa kipande cha ardhi watakapokusanyika na kuishi ili kuzuia uvamizi wa ardhi za kibinafsi na umma,” alisema Thoya.

Kwa sasa Thoya amependekeza kuwepo kwa mazungumzo ya maelewano kati ya wamiliki wa ardhi na maskwota ili kupata suluhu ya kudumu na kumaliza tatizo la uskwota kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani.