Share news tips with us here at Hivisasa

Kuchupuka kwa maswala ya itikadi kali, ugaidi na uhalifu duniani kumechangiwa na tofauti za kidini, hivyo basi kuna haja ya watu kupata ufahamu kuhusiana na dini mbalimbali ili kuzuia ugaidi.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Global Peace Foundation nchini Daniel Juma Omondi ameyasema hayo katika mkutano na wanahabari wakati wa kujadili maswala ya kusitisha itikadi kali, ugaidi na uhalifu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Omondi alisema kuwa kuna haja ya watu kuwa na uelewano kama jamii moja, licha ya kuwepo na dini tofauti ili kuona kwamba wanaishi kwa amani huku akielezea matumani ya kudhibitiwa kwa visa vya kigaidi.

“Iwapo jamii itakuja pamoja na kushirikiana vyema, basi uelewano wa kidini utakuwepo katika kali ya watu na maswala haya basi tutaweza kuyadhibiti ili ulimwengu huu kuwa wa amani,” alieleza Omondi.

Mwanaharakati huyo aliahidi kuihamasisha jamii ulimwenguni kwa kutumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa maswala ya usalama yanaangaziwa vyema na watu wanaisha kama jamii.