Chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut tawi la Mombasa kimeionya vikali Tume ya kuajiri walimu nchini TSC dhidi ya kuwalizimisha walimu kukubali kutia saini kandarasi ya utendakazi.
Kulingana na Katibu wa chama hicho katika Kaunti ya Mombasa Dan Aloo, maafisa wa TSC katika kaunti hiyo wameonekana kwa kiwango kikubwa kuwalazimisha walimu kukubali kandarasi hiyo bila ya kuwafahamisha umuhimu na athari zake.
Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Aloo alisema kuwa kama chama cha kutetea maslahi ya walimu, kamwe hawatakubali kuona walimu wakikandamizwa na serikili pamoja na waajiri wao.
Aloo alisema kuwa watahakikisha kuwa walimu hawakubali kandarasi hiyo bila ya vigezo muhimu kujadiliwa na kuafikiana vyema, na iwapo watalazimishwa kutia saini kandarasi hiyo, basi wataandaa mgomo kwani katiba imewapa uhuru huo.
“Tungependa kuwambia maafisa wa TSC kutowalazimisha walimu kukubali kandarasi hiyo kabla ya kuelezewa bayana umuhimu wake,” alisema Aloo.
Katibu huyo wa Knut aliahidi kuwashauri walimu kutokubali mpango huo wa serikali na TSC kwa kudai kuwa lengo lao kuu ni kuvuruga chama cha walimu nchini Knut.