Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Tume ya kitaifa ya ardhi imeahidi kutoa uamuzi kuhusiana na wakazi watakaofidiwa na serikali kufuatia kuathirika na miradi iliyozinduliwa na serikali ya ujenzi wa barabara ya reli ya kisasa na ile ya Dongo Kundu.

Naibu Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Abigael Mbagaya amesema kwamba tume hiyo inafuatilia kwa makini ukaguzi wa ardhi zitakazotumika na serikali kwa miradi hiyo na jinsi watakavyowalipa fidai wenyeji.

Akiongea na wanahabari baada ya kufanyika kwa vikao vya ardhi na wakazi wa Mombasa katika ukumbi wa taasisi ya mafunzo ya serikali GTI mjini Mombasa siku ya Jumanne, Bi Mbagaya alisema kwamba miradi hiyo ya serikali ni muhimu kwa taifa hili, na lazima kwa wakazi watakaoathirika kufika mbele ya vikao hivyo ili kusitisha malumbano.       

Alisema kwamba iwapo wanaodai kuathirika na miradi hiyo hawatafika mbele ya vikao hivyo kutatua mzozo uliopo, basi tume hiyo itatoa maamuzi yake kulingana na stakabadhi zinazowalishwa kwao ili miradi hiyo ya serikali kutekelezwa.

"Kama tume tunawasihi wakazi walio na malalamishi kufika mbele ya vikao hivyo na kutoa stakabadhi zao na malalamishi yao ili tujue vipi tutamaliza mzozo ya ardhi, na iwapo wakazi watapuuza, basi sisi tutawalipa fidia wale watakaotueleza vyema na kufanya ukaguzi wa kina na miradi ya serikali iendelee," alisema Mbagaya.

Wakati uo huo, amepinga madai yanayotolewa na wakazi kwamba tume hiyo inatoa fidia kwa watu wasiokuwa wamiliki halali wa ardhi hizo, na akasema kwamba sheria za utowaji fidia zimezingatiwa na kwame hakuna muathiriwa atakayetengwa.

Kikao hicho, ambacho ni cha mwisho, kinalenga kutoa uamuzi ya watu watakaofidiwa na serikali ili kuzuia mzozo ya ardhi wakati miradi hiyo inatekelezwa.