Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameshauri tume ya kusimamia vyuo vikuu nchini kuhusisha washkadau wote wa elimu kwa jambo lolote wafanyalo kabla ya kuamua la kufanya ili kuonyesha uwazi na haki kwa wananchi.
Hii ni baada ya tume hiyo kuagiza kufunga mabewa 10 ya chuo kikuu cha Kisii kwa siku 90 zijazo kwa kile kilichosemekana kuwa chuo hicho hakijaafikia mahitaji yale yanastahili kimasomo, huku Gavana Nyagarama akisema tume hiyo haikufuata utaratibu kabla ya kutoa agizo la kufunga baadhi ya mabewa hayo.
Kulingana na Nyagarama, tume hiyo haikuhusisha washkadau wote wa elimu kabla ya kutoa maamuzi ya kutaka baadhi ya mabewa ya chuo hicho cha Kisii na kusema hiyo si haki.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika sherehe ya mazishi iliyoandaliwa katika eneo la Nyainogu, Nyagarama aliomba tume hiyo kuhusisha washikadau wa elimu kabla ya kutoa uamuzi wowote ili kuonyesha haki kwa wananchi wa Kenya.
“Naomba tume ya CUE kuhusisha washkadau wote wa elimu kabla ya kufanya jambo lolote ili kuonyesha haki na uwazi kwa wanachi,” alisema Nyagarama.
Aidha, Nyagarama alisema kama viongozi hawatakubali mabewa ya chuo kikuu cha Kisii kufungwa kamwe na kusema kuwa watajaribu kila wawezalo kuhakikisha wanafunzi hawataathirika kimasomo.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o ambaye alisema mabewa ya chuo kikuu cha Kisii hayafungwi.