Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Rongai Raymond Moi ametakiwa kutumia fedha za hazina ya ustawishaji eneo bunge lake, CDF, kujenga kituo cha polisi katika kituo cha kibiashara cha Moricho, ili kukabiliana na uhalifu eneo hilo.

Wito huo unajiri juma moja tu baada ya wazee wa nyumba kumi kuvaamiwa na wapishi wa pombe haramu eneo hilo la Moricho, kwa madai ya kuhangaisha biashara yao.

Wakizungumza na mwandishi huyu Jumatatu, baadhi ya wakaazi hao walisema visa vingi vya uhalifu haviripotiwi kwa polisi, kwani kituo kilicho karibu nao kimo zaidi ya kilomita 20.

“Pombe haiwezi kumalizwa kama hatutaletewa kituo cha polisi hapa, na tupewe maafisa wa polisi ambao hawatahongwa na wapishi hawa wa pombe haramu. Hata wizi ukitokea hakuna polisi wa kuita, kwa sababu walio karibu wako Rongai mjini,” alisema William Chirchir Kiplagat.

Wenzetu wa Lenginet, Mogoiwet, Kapsetek, Burgei na Mawe pia hawana vituo vya polisi, kwa hivyo hapa kwetu tukijengewa kituo cha polisi, itakuwa afueni kwao pia,” alisema mkaazi Daniel Cherono.

Mwanzoni wa mwaka huu, mbunge Raymond akizungumza katika kituo cha kibiashara cha kampi ya Moto, alisema ofisi yake itashirikiana na idara zingine za kiserikali kufadhili ujenzi zaidi wa vituo vya polisi eneo bunge hilo, ili kukabiliana na wezi wa mifugo.