Shughuli katika kituo cha Huduma Centre Kaunti ya Mombasa huenda zikaimarika zaidi baada ya serikali kusema kuwa ina mpango wa kukipanua zaidi.
Kituo hicho ni moja kati ya vituo vingine nchini ambavyo vilianzishwa na serikali kuu ili kurahisisha utoaji wa stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho na kadhalika.
Akiongea na waandishi kituoni humo siku ya Jumatatu, waziri wa utumishi wa umma Bi Cecily Kariuki alisema kuwa serikali inafahamu changamoto zinazoshuhudiwa katika kituo hicho na kusema kwamba wanashughulikia jambo hilo.
“Hiki ni kituo ambacho kinashuhudia idadi kubwa ya wateja na nimesikia malalamiko ya wananchi. Tuna mpango wa kupanua sehemu hii,” alisema Kariuki.
Waziri huyo aliyezuru kukagua kituo hicho kinachotoa zaidi ya huduma 30 pia amewasihi wananchi kuwa watulivu kila kunapokuwa na hitilafu ya kimitambo.
“Wakati mwingine huduma zinaendeshwa polepole kutokana na hitilafu kwenye tarakilishi zetu na kunakuwa na msongamano. Hiyo ni kawaida na tunafaa kuwa watulivu,” alisema Kariuki.
Hata hivyo wananchi waliyoongea na mwandishi huyu walipongeza hatua hiyo ya serikali ya kuanzisha kituo hicho na kusema kuwa kimerahisisha mambo mengi sana.
“Hapo mwanzo tulikuwa tukihangaika sana. Kila stakabadhi unatafuta sehemu tofauti lakini hapa unapata kila kitu mahali pamoja,” alisema mteja mmoja.