Kulikuwa na kisanga katika uwanja wa michezo wa manispaa ya mji wa Naivasha Jumatatu baada ya wafanyikazi katika sekta ya maua kuzozana kuhusu mbinu ya uchaguzi wa wasimamizi wa chama chao cha Kenya Plantations and Agricultural Workers Union.
Wakati wa tukio hilo, wengi walikuwa wamejibizana kabla ya afisaa msimamizi wa maswala ya leba wilayani Naivasha Elizabeth Kamau kuingilia kati na kuwatuliza.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, huku Justus Ekino akichaguliwa kama mwenyekiti wa chama hicho tawi la Naivasha.
Akizungumza pindi tu baada ya uchaguzi huo Ekino ametoa ilani kwa kampuni tele za maua ambazo hadi wa sasa zinakandamiza haki za wafanyikazi wao kwa kuwalipa mishahara midogo.
Naye katibu wa chama hicho Ferdinand Juma amesema kuwa kampuni hizo hazikuwa zimetekeleza makubaliano mapya na kukosa kuwalipa wafanyikazi mishahara inayostahili na kuongeza kuwa tukio hilo litaangaliwa kikamilifu.
Kwa upande wake Bi Kamau amesema kuwa waliochaguliwa watashirikiana na afisi yake ili kuona kuwa maswala ya wafanyikazi yametiliwa maanani.