Uhaba wa maji umeripotiwa kuzikumba baadhi ya sehemu mjini Mombasa, ambapo kwa siku mbili sasa wakazi wanalazimika kuyatumia maji ya chumvi kufuatia ukosekana kwa maji safi.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu wanahofia kuwa huenda kukazuka magonjwa kama kipindupindu kutokana na hali ya maji wanayotumia kwa sasa.
kwa mjibu wa mmoja wao aliyetambulika kama mama Rose, kwa kawaida huwa wananunua maji safi shilingi kumi kwa mtungi mmoja, ila kwa sasa wanauziwa mtungi mmoja wa maji ya chumvi kwa shilingi ishirini.
Inadaiwa huduma ya maji mjini humo imesitishwa kufuatia tofauti baina bodi ya maji eneo la Pwani na kampuni ya maji ya Mombasa Water kutokana madeni ya mabilioni ya pesa.
Hadi tukiandika taarifa hii, pande zote mbili hazikua zimetoa taarifa zozote kuhusiana na tatizo hilo, na sasa wakazi wanaitaka serikali ya kaunti kutatua shida hiyo.