Uhifadhi wa Ziwa Naivasha, ambalo sasa linakaabiliwa na changamoto ya kuenea kwa mmea wa gugu maji, hautafaulu iwapo unyakuzi wa ardhi ya ziwa hilo hautaangaziwa kwa dharura.
Afisa msimamizi wa muungano wa watumizi wa raslimali za maji mjini Naivasha David Kihagi amekemea vikali unyakuzi wa ardhi inayozunguka ziwa hilo, iliyotengewa maswala ya uhifadhi wake.
Shirika hilo limesema kwamba inashangaza jinsi wanyakuzi wa ardhi hiyo walivyojipatia hati miliki za mashamba yaliyonyakuliwa, huku akikiri kwamba kuwatoa kwenye ardhi hiyo imekuwa kibarua kigumu.
“Harakati za walinda mazingira eneo hili zimeambulia patupu kwa sababu tumewekewa kikwazo na wanyakuzi hao” alisema Kihagi.
Kulingana na Kihagi, uhifadhi wa Ziwa Naivasha ni zoezi la kila mshikadau, ikiwemo serikali kuu, ile ya Kaunti ya Nakuru, wavuvi pamoja na wananchi.
Wakazi wanaoishi katika maeneo yaliyokaribu na Ziwa Naivasha ikiwemo vyanzo vya maji ya mito inayoelekea humo, wameanza kupokea mafunzo ya jinsi ya kulinda mazingira kutoka kwa shirika moja lisilo la kiserikali la WWF kwa ushirika wa LANARUA.
“Mafunzo tunayowapa ni jinsi ya kujiepusha na kilimo kinachosababisha mmomonyoko wa udongo, ambao unabebwa na maji hadi Ziwani Naivasha na hatimaye kuathiri sio tu samaki na wanyama wengine, bali pia kuhatarisha maisha ya wavuvi wanaokwama kwenye magugu maji,” aliongeza.