Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana elfu tatu wanaendelea kufaidi katika miradi ya hamasa na kutoa habari kwa maafisa wa usalama baada ya ushirikiano baina ya maafisa wa usalama na vijana kuimarika katika Kaunti ya Mombasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu wa shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre Phylis Muema alisema kuwa ushirikiano huo umefaulu na kupelekea vijana kujiunga katika makundi ya kijamii ya usalama katika mitandao, na kutoa ripoti kwa maafisa wa usalama.

Aidha, Muema alisema kuwa ushirikiano wa jamii na maafisa wa usalama utaendeleza kupunguza visa vya vijana kujiunga na makundi ya kigaidi na ufisadi miongoni mwa maafisa wa usalama katika Kaunti ya Mombasa.

Wakati huo huo, katibu mpangaji katika muungano wa vyuo na taasisi mkoani Pwani Abubakar Swabir ametoa wito kwa vijana kujisajili kama wapiga kura ili kuweza kupata viongozi wa sawa katika maeneo ya Mombasa ifikapo wakati wa kupiga kura.

Kulingana na Abubakar, jamii katika maeneo ya Pwani haijatambua umuhimu wa kujisajili.

Katibu huyo alisisitiza kuwa ni lazima kwa wakazi kuhamasishwa ili kutambua jukumu hilo.

Kwa mtazamo wake, jamii imezoea kupokea pesa kutoka kwa wanasaisa ili kujisajili katika maeneo mbali mbali, na kutotambua umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura bila malipo na kufaidi miradi ya ugatuzi nchini.