Share news tips with us here at Hivisasa

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imesema kuwa wakaazi wengi katika kaunti ya Nakuru hukosa kujisajili kwa kukosa ufahamu juu ya umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura.

Mshirikishi wa tume hiyo katika eneo la kati mwa bonde la ufa David Towet amesema kuwa wakaazi wengi haswa walio katika sehemu za mashambani hawajatambua umuhimu wa kuisajili kama wapiga kura.

Akiongea mjini Nakuru wakati wa shughuli ya kuwahamasisha wanahabari juu ya uandikishaji wapiga kura,Towet alisema kuwa idadi kubwa ya watu waliofikisha umri wa kujiandikisha wangali kufanya hivo.

Alisema kuwa hali hiyo inaathiri dhamira ya IEBC ya kuwaandikisha zaidi ya wapiga kura milioni kumi na nane.

“IEBC ina kila lengo la kuandikisha wapiga kura wengi zaidi lakini wengi wa watu haswa hapa Nakuru hawana ufahamu kuhusu umuhimu wa kujiandikisha na kwa hivyo hawajachukua jukumu la kufanya hivyo,” Towett alisema.

“Kama tunaweza kuwafahamisha hawa watu kuhusu shuguli ya kujiandikisha na umuhimu wake basi wataweza kujiandikisha na tutakuwa na wapiga kura wengi sana katika kaunti ya Nakuru,”aliongeza.

Towet aliongeza kuwa tume hiyo itafanya kila juhudi kuwafikia wapiga kura wengi zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja ujao ili waweze kujisajili kama wapiga kura.

“Tutazunguka kila mahali haswa mashinani ili tuweze kuwapa nafasi watu wengi zaidi wanaotaka kujiandikisha,” alisema.