Share news tips with us here at Hivisasa

Mizozo ya unyakuzi wa ardhi imetajwa kuongezeka kwenye mpaka wa Kaunti za Mombasa na Kwale.

Akizungumza na wanahabari katika chuo cha mafunzo ya kiserikali cha Matuga siku ya Jumanne, Mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya ardhi Dkt Mohamed Swazuri, alisema kuwa mizozo hiyo inaendelea kuongezeka huku wananchi walio wenyeji wa sehemu hizo wakikosa hatimiliki za ardhi.

Swazuri alisema kuwa wengi wanaodai kumiliki ardhi za eneo hilo sio wenyeji wala wazawa wa eneo hilo, na pia hawaishi katika maeneo hayo.

Swazuri alisema tume hiyo imebaini kuwa wenye hatimiliki za ardhi za eneo hilo sio wenyeji suala alilotaja kusababishwa na dhulma za kihistoria.

Aidha, alisema kwamba swala hilo la ardhi katika eneo la Pwani lingepata suluhu iwapo sheria ya dhulma za kihistoria ingepitishwa, huku akiwataka wabunge kuipitisha sheria hiyo ili kusaidia kutatua tatizo sugu la ardhi.