Ripoti zinaonyesha visa vya dhuluma na unyanyasaji wa kijinsia vimekithiri katika kaunti ya Mombasa.
Haya ni kulingana na mratiba wa shirika la maendeleo ya wanawake eneo la Pwani Tom Ng'ar.
Katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu siku ya Jumamosi katika hafla ya kuyahamasisha makundi ya wanawake na vijana dhidi ya dhuluma na unyanyasaji wa kijinsia huko Mshomoroni, Ng'ar amesema visa hivyo vimekithiri katika maeneo ya Kisauni, Changamwe na Likoni.
Visa hivyo vimetajwa kuwa ubakaji na mizozano katika ndoa inayosababisha wanandoa kujeruhiana hata kuuwana.
Kwa upande wake mzee wa mtaa wa eneo la Bengala ulioko Mshomoroni David Chaka aliwalaumu baadhi ya wazazi katika sehemu hiyo kwa kunyamazia uovu unapotendeka.
Aidha, alitoa changamoto zake kwa viongozi katika eneo hilo kushughulikia swala hilo ambalo limekuwa donda ndugu katika jamii.