Shirika la kitaifa la huduma kwa vijana NYS limesema kuwa zoezi la kuzindua upya miradi hiyo litaanza katika Kaunti ya Mombasa kabla kuelekea maeneo mengine nchini.
Shirika hilo ambalo lilikumbwa na misukosuko katika siku za hivi majuzi kutokana na visa vya ufisadi limepanga kuzindua upya miradi yake na kusajili vijana zaidi hivi karibuni.
Akiongea katika soko la Kongowea siku ya Jumamosi wakati wa zoezi la usafi sokoni humo, mkurugenzi wa shirika hilo Richard Ndubai aliwaambia vijana kuwa hii ni fursa kubwa kwa vijana wa Pwani.
“Nyinyi mna bahati sana kwa sababu serikali imepanga kwamba uzinduzi huo utaanzia Mombasa na utafanyika katika soko hili la Kongowea,” alisema Ndubai.
Ndubai pia aliwasihi vijana nchini kutia bidii na kutumia fursa ya shirika hilo kujiendeleza kimaisha na kuepuka mambo yasiyofaa katika jamii.
Shirika hilo pia limewataka vijana kutumia vyema fedha watakazokuwa wakilipwa na kuwekeza katika biashara, ambapo kila mmoja atakuwa akilipwa shilingi 571.
“Tunataka vijana wetu wabadilike na tuna imani kwamba NYS itasaidia vijana wa humu nchini ambao hawana ajira,” alisema Ndubai.
Vijana waliojitokeza katika hafla hiyo ya Jumamosi walijumuika pamoja katika uzinduzi wa zoezi la usafi katika soko hilo ambalo hutegemewa zaidi na wakaazi kutoka maeneo mbalimbali ya Pwani.
Mbunge wa Nyali Hezron Awiti aliyeandamana na mkurugenzi huyo wa NYS pia aliunga mkono mpango huo na kuahidi kuwa ataendelea kuhakikisha kuwa vijana wanabadilisha maisha yao.