Viongozi wa kisiasa wa mrengo wa Jubilee mjini Mombasa, wameapa kuwaongoza wakaazi katika maandamano na kuling’oa bango lenye nembo ya Fidel Odinga, iwapo barabara mpya iliyopewa jina la marehemu mwanawe Raila Odinga haitabadilishwa jina.
Wanasiasa hao wameitaja hatua ya serikali ya Kaunti ya Mombasa kulibadili jina la barabara ya ‘New Nyali Road’ na kuiita ‘Fidel Odinga Road’ kama inayowakosea heshima vigogo na watu mashuhuri wazaliwa wa eneo la Pwani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano muda mchache baada ya barabara hiyo kuzinduliwa na kinara wa Cord Raila Odinga, mwenyekiti wa TNA Mombasa, Matano Chengo, alikashifu uzinduzi huo na kusema kuwa kuna watu wanaofaa kupewa jina la barabara hiyo.
Chengo alisema kuwa watu kama Mekatilili wa Menza na aliyekuwa mhadhiri wa chuo kikuu marehemu Ali Mazrui, ni miongoni mwa watu ambao wanastahili kutambuliwa badala ya marehemu Fidel Odinga.
“Marehemu Fidel aliifanyia nini Mombasa kimo cha barabara kupewa jina lake? Tunaitaka serikali ya kaunti kubadilisha jina hilo mara moja kabla hatujachukua hatua na kuliong’oa bango hilo,” alisema Chengo.
Kauli ya Chengo imeungwa mkono na seneta mteule wa Kaunti ya Mombasa, Emma Mbura, ambaye katika kikao na wanahabari mjini Nairobi siku ya Jumatano, aliitaja hatua hiyo kama ya kejeli kwa wakaazi kwa wa Pwani.
Siku ya Jumatano, kinara wa Cord Raila Odinga, aliwaongoza viongozi mjini Mombasa, katika uzinduzi wa bara ya Fidel Odinga, ambayo itakua kama kumbukumbu kwa marehemu Fidel Odinga aliyefarika mapema mwaka jana.
Hii ilikuwa ni hitimisho la ahadi iliyotolewa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, wakati wa mazishi wa marehemu Fidel mwaka uliopita.