Share news tips with us here at Hivisasa

Vyuo vikuu vya umma nchini huenda vikapata pigo kubwa baada ya waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i, kutangaza kuwa serikali imefikia uamuzi wa kutoruhusu vyuo vya umma kujenga vyuo tanzu zaidi nchini, kama inavyoshuhudiwa kwa sasa.

Akizungumza siku ya Jumanne katika uzinduzi wa msingi wa utafiti wa uhandisi, Matiang'i vile vile alivionya vyuo vya umma dhidi ya kuchukua mikopo ambayo mwishowe vinashindwa kulipa kwa madhumuni ya kufadhili vyuo tanzu.

Aidha, alitoa tahadhari pia kwa vile vyuo ambavyo vinachukua wanafunzi walio na alama za chini kwa minajili ya kutafuta pesa.

Waziri huyo alisema kuwa uamuzi huo umeafikiwa kutokana na haja ya kulinda uadilifu wa vyuo humu nchini.

Kutokana na hilo, kamati ya vyuo vya juu haitaruhusiwa kutoa leseni kwa chuo chochote cha umma nchini kwa madhumuni ya kujenga chuo tanzu.