Wafanyikazi-vibarua kadhaa katika kiwanda cha kutengeneza unga cha Mombasa Maize Millers wamerejeshwa nyumbani kutokana na kile kinachotajwa kama utovu wa nidhamu kazini.
Vibarua hao wanadaiwa kuzua fujo siku ya Ijumaa kiwandani humo walipokuwa wakiwatetea wenzao waliokuwa wameamrishwa kwenda nyumbani baada ya usimamizi wa kiwanda hicho kudai kwamba hawafuati sheria za kazi.
Kisa hicho cha Ijumaa kilipelekea vibarua wote wanaofanya kazi kiwandani humo kufurushwa na kubakishwa wale walioajiriwa rasmi kendelea na kazi.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumamosi, mmoja wa walinzi alisema kwamba vibarua hao walianza fujo huku wakitoa cheche za matusi, jambo liliowafanya kuitisha msaada kutoka kwa walinzi wengine.
“Walianza fujo wakiwatetea wenzao wawili waliokuwa wamelazimishwa kwenda nyumbani kwa kukosa kufuata sheria, hapo ndipo wenzao walipozua, ilibidi tuwaite walinzi wengine kutoka nje watusaidie,” alisema mlinzi huyo.
Inadaiwa kwamba vibarua hao wamekuwa na tabia ya kutozingatia saa za kuingia kazini, jambo linalolemaza utaratibu wa kazi.
Hata hivyo baadhi yao walirudi tena asubuhi ya Jumamosi lakini wakazuiliwa mlangoni kwani walinzi hao walikuwa wameamrishwa kufanya hivyo.