Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kundi la vijana lililo chini ya shirika la kitaifa la huduma kwa vijana nchini NYS liliandamana katika barabara za mjini Nakuru siku ya Alhamisi likimuunga mkono waziri wa ugatuzi Anne Waiguru na  kusema kwamba vijana wa Kenya walikuwa wametengwa na serikali za hapo awali.

Vijana hao waliokuwa wamebeba mabango wakionyesha kumuunga mkono Waiguru waliandamana hadi kwenye mtaa wa Langalanga ulio viungani mwa mji wa Nakuru, huku wakishutumu viongozi wa mrengo pinzani na kundi la wanachama wa muungano wa Jubilee wakisema wametia siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

John Njoroge, mmoja wa vijana walioandamana ambaye pia ni mkaazi wa eneno la Mwariki alilalama kwamba vijana hapa nchini walikuwa wametengwa na serikali tatu za hapo awali, lakini chini ya serikali ya Jubilee, wamepewa kipau mbele.

Aliongeza kwamba shinikizo zinazotolewa kuhusiana na Waiguru hazielekezwi tu kwake bali pia kwa vijana wa wakenya ambao kwa sasa wanaweza kukimu mahitaji yao kifedha kupitia kwa fedha wanazopata kutoka kwa mradi wa NYS.

"Changamoto ambayo ningependa kuipa serikali yetu ni kwamba Wakati Waiguru anaposhtumiwa, sio yeye pekee anayeshutmiwa bali ni vjana wanashutumiwa. Hii ni kwa sababu vijana hawajashughulikiwa na serikali za hapo awali, lakini Waiguru alipoanza kushughulikia vijana, mambo ya madawa ya kulevya yaliisha," alidokeza Njoroge.

Kijana mwingine kwa jina la Peter Kimani, ambaye pia amefaidika kutokana na mradi huo wa NYS alishutumu wanaomtaka waiguru kujiuzulu, na kusema kuwa ni kumwonea kijicho waziri huyo.

"Waziri Waiguru wakati alionekana anafanya kazi, watu walianza kumtafutia fitina wakisema yeye ni mfisadi, wengine wakidai anatumia fedha za vijana na pia mali ya serikali. Hayo mambo yote ni ya uongo. Tunaamini wale wote wanaompiga vita waziri huyo wanampiga kwa njia ya kisiasa kwa sababu walikuwa kwenye hii serikali kwa miaka mingi na hawakufanya lolote," aliongezea.

Maeneo bunge ya Nakuru Mashariki na Magharibi yaliajiri vijana 1,350 na 1,300 mtawalia chini ya huduma ya kitaifa ya Vijana NYS.