Viongozi wa vijana Naivasha wameonyesha hofu yao baada ya kubainika kwamba vijana elfu kumi hawana vitambulisho vya kitaifa.
Katika kikao na wanahabari Anthony Rebo kiongozi wa vijana eneo hilo anasema kuwa hatua hio ni kutokana na kujikokota kwa shughuli ya kutoa vitambulisho.
"Wafanyikazi wa kuhudumu katika afisi za kutoa vitambulisho ni wachache na inafanya shughuli hio kuendeshwa kwa upole mno," alisema Rebo.
Kwa mujibu wake waathiriwa zaidi ni vijana wa Mai Mahiu waliokamilisha sekondari miaka miwili iliyopita.
Ni kutokana na hilo ambapo ametoa wito kwa usimamizi wa kaunti ya Nakuru kutatua suala hilo.
"Naomba viongozi wa kaunti waingilie kati suala hili ili vijana pia washiriki katika maamuzi muhimu nchini," aliongeza Rebo.
Na huku tukikaribia uchaguzi mkuu 2017, Rebo alitoa wito kwa serikali kutenga fedha zaidi kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake.
"IEBC inafaa kuongezwa fedha za kusimamia shughuli ya kusajili wapiga kura," aliongeza Rebo.
Amewataka vijana kuepuka machafuko.