Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana katika Kaunti ya Kisii wameshauriwa kutotegemea kazi za ajira na badala yake kukumbatia kilimo na biashara ili kujiendeleza kimaisha.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya vijana katika sehemu mbalimbali humaliza masomo na kusalia nyumbani wakisubiri kazi za ajira kutolewa na serikali pamoja na mashirika mengine.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii, mkurugenzi wa vijana katika Kaunti ya Kisii Douglas Arege aliomba vijana kukumbatia kilimo na biashara ili kujipatia riziki ya kila siku na kujikimu kimaisha badala ya ya kutegemea kazi za ajira.

Kulingana naye, serikali haiwezi kuajiri kila mtu kwani nafasi za ajira ni chache ikilinganishwa na wasomi humu nchini.

Arege alisema kuwa vijana wengi wamejiendeleza kupitia biashara na kusema wafanyibiashara ni miongoni mwa watu ambao ni tajiri katika taifa la Kenya.

Aliomba vijana kukumbatia biashara pamoja na kilimo kwa moyo mmoja ili kujinufaisha.

“Vijana wengi wamesoma na wanasubiri kupata ajira katika mashirika ya kiserikali. Nawaomba waanze kilimo na wajihusishe na biashara ili wajiendeleze kimaisha,” alisema Arege.

Arege alisema vijana wanapojihusisha na biashara hujua mengi na huweza kuwa viongozi badala ya kukaa nyumbani bila kufanya lolote.