Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la vijana wa huduma kwa taifa (NYS) litawaajiri vijana zaidi kutoka Wadi ya Biashara kushiriki katika shuguli za kusafisha mitaa mwaka ujao.

Kulingana na mwakilishi wa wadi hiyo Stephen Kuria, Wizara ya Ugatuzi imemuhakikishia kuwa vijana zaidi kutoka eneo hilo wataajiriwa na NYS katika awamu ya pili itakayo anza mwezi Feburari 2016.

Akiongea siku ya Alhamisi alipoyakabidhi makundi ya vijana hundi katika afisi yake, Kuria alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa idadi ya vijana wasio na kazi imepunguka katika eneo hilo.

“Mwaka ujao tutahakikisha kuwa vijana wengine wamechukuliwa kufanya kazi za NYS kwa sababu nimeongea nao na wamenihakikishia kuwa hatutaachwa nje ya shughuli hiyo awamu ya pili itakapoanza,” alisema Kuria.

Kuria alitoa wito kwa vijana kutodharau kazi hiyo ya kusafisha mitaa na kusema kuwa iwapo kazi hiyo si ya kuridhisha, cha muhimu ni kipato wanachopata.

“Tusibague kazi hiyo na tujitokeza kuifanya tutakapoitwa kwani pesa mutakazo pata zitakuwa za manufaa kwenu,” alisema Kuria.

Aidha, aliwata vijana kutumia pesa wanazopata kufungua miradi midogo midogo ya maendeleo na kujiepusha kutumia pesa hizo kwa anasa na starehe.

“Hiyo kazi ni ya muda tu na kama hamtatumia pesa hizo vizuri, basi nyinyi wenyewe ndio mutajilaumu. Ni vyema muweze kufungua biashara ili muweze kujitegemea siku za usoni,” alisema Kuria.