Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wazazi katika eneo la Likoni wamelalamikia hatua ya vijana wengi kuonekana kukumbatia biashara ya pikipiki al maarufu bodaboda.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, wazazi hao walielezea wasiwasi wao kuwa watoto wao wa kiume wameanza kukataa shule ili kuanza biashara hiyo, hali ambayo walidai imechangia ongezeko la ajali za barabarani.

Halima Ali, mzazi, alisema kuwa mwanawe wa kidato cha pili alikataa kwenda shule huku akidai kuwa atapata pesa kwa kuendesha pikipiki.

Akizungumza na mwandishi huyu katika eneo la Kiwerera, Ali Karisa, mzazi, alisema kuwa mwanawe mwenye umri wa miaka kumi na nane sasa ameifanya kazi hiyo kwa miaka mitatu, tangu alipoacha shule.

"Alikuwa hapati chochote shuleni na aliponiambia kuwa anataka kufanya kazi ya bodaboda, niliona kama amesema jambo la busara," alisema Ali.

Huku kila mzazi akitoa sababu zake za kukumbatia au kukashifu biashara hiyo, vijana wengi wadogo hasa katika eneo la Likoni wamekumbatia biashara hiyo huku wakisema kuwa inawasaidia kujiepusha na utumizi wa dawa za kulevya.

"Mimi niliamua kuacha shule na kujitosa katika biashara hii kwa sababu ya changamoto za kimaisha. Biashara hii ina hatari zake lakini kuishi lazima," alisema Abubakar, mhudumu wa bodaboda.

Aliongeza, "kwa kweli kila mmoja ana sababu ya kufanya jambo maishani lakini nawahimiza vijana wenzangu kusoma kwanza kwani haya maisha ni magumu."