Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa Afiya Rama amesema kuwa hatua ya vijana kujitosa katika utumizi wa mihadarati na uhalifu imetokana na vijana hao kutojishughulisha na miradi ya kimaendeleo.

Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatano, Rama alisema kuwa vijana hao wanadai kuwa kujitosa kwao kwa utumizi wa mihadarati na uhalifu umechangiwa na ukosefu wa ajira ilhali wengi wao hukwepa ushauri wa kijamii na kusalia maskani.

Alisema kuwa chama hicho kimejitolea kikamilifu kuhakikisha kuwa vijana wanajinasua kutoka jinamizi hilo na kupata matibabu maalum ili kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kujikimu kimaisha.

"Tumejitolea kikamilifu kuhakikisha kuwa vijana wanajinasua kutoka jinamizi hilo la mihadarati na uhalifu ili kuona kuwa wanajishughulisha na masuala ya kimaendeleo mashinani," alisema Rama.

Bi Rama aliwakosa viongozi wa kisiasa wanaochangia vijana wengi kujihusisha na uhalifu, kutokana na madai kuwa wanawafadhili kuzua vurugu.

Aliahidi kuzuru mashinani na kuwasaidia vijana katika kuwahamasisha kuhusu masuala muhimu ikiwemo ya kimaendeleo na jinsi ya kuboresha maisha yao katika siku za usoni.