Vijana kutoka eneo la Mombasa wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa masuala yenye faida na umuhimu katika maisha yao, badala ya kuitumia kwa njia ambazo zinaathiri mwelekeo mzima wa taaluma zao maishani.
Akizungumza siku ya Jumapili katika mkahawa wa Sarova WhiteSands Resort kwenye mahojiano na mwandishi huyu, Abubakar Swabir, anayepania kujimwaya kwenye siasa za kupigania kiti cha useneta katika Kaunti ya Mombasa, alisema kuwa wengi wa vijana hasa kutoka maeneo ya Pwani wamekuwa wakitumia mitandao kwa njia za kujifunza masuala ya uhalifu na kuwa na itikadi potovu.
Alisema kuwa hali hiyo imechangia vijana wengi kujiunga na magenge ya uhalifu.
Swabir alisema kuwa sasa wamejiunga na shirika la Brave kuwafadi vijana kwenye ushauri, na kutoa wito kwa wazazi pamoja na jamii kwa jumla kushikana mikono ili kuhakikisha kuwa vijana ambao wameathiriwa na masuala ya itikadi kali wanawiana na jamii ili kuendeleza nchi na kuishi maisha ya sawa.
“Ni nafasi yetu kama jamii kuanza kuangalia na kutumia mitandao vizuri. Serikali yapaswa kutoa mwelekeo au kufunga baadhi ya tovuti ambazo zinaeneza itikadi kali,” alisema Swabir.
Shirika hilo la Brave liko kwenye harakati za kuwafikia vijana na jamii kwa jumla kwa majuma matatu ili kueneza ujumbe huo wa jinsi ya kujiepusha na matendo mabaya na kufanya miradi ya kuwafaa kiuchumi.