Mwakilishi mteule katika bunge la Kaunti ya Nakuru Bi Rosemary Okemwa ametoa wito kwa vijana kumakinika na kutumia muda uliosalia kujisajili kama wapiga kura.
Akizungumza katika kituo kimoja cha usajili wa wapiga kura siku ya Jumatatu, Okemwa ambaye ametangaza azma ya kuwania kiti cha wadi ya Biashara, alisema kuwa kila kijana anafaa kujisajili kama mpiga kura.
"Vijana ni nguzo muhimu kwa taifa hili na mimi nawarai kujisajili kama wapiga kura kwa wingi ili tufanye maamuzi bora," alisema Okemwa.
Wakati huo huo, amewataka vijana kuripoti visa vyovyote vya changamoto wanazokumbana nazo katika vituo vya usajili ili vishughulikiwe.
Mwakilishi huyo mteule wa wadi ameapa kushirikiana na vijana na akina mama ili kuinua maisha yao.