Vijana Pwani wamehimizwa kutojihusisha na makundi yanayolenga kuvuruga amani katika eneo hilo na badala yake washirikiane na maafisa wa usalama ili kusaidia kuimarisha usalama nchini.
Akizungumza kwenye kongamano lililowaleta pamoja vijana wa ukanda wa Pwani mjini Mombasa siku ya Jumatatu, afisa mratibu wa mipangilio katika shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, Francis Gamba, alisema kuwa wakati umefika kwa vijana wa ukanda huo kuyaangazia masuala yatakayo wafaidi maishani badala ya kukubali kutumiwa na wanasiasa.
“Vijana tusikubali kutumiwa na mtu kwa maslahi yake ya kibinafsi. Leo hii ukitiwa nguvuni utakua pekee yako. Tufanye kazi pamoja na serikali tuinue uchumi wa taifa ili tujiendeleze kimaisha,” alisema Gamba.
Aidha, mwanaharakati huyo wa haki za binadamu alisema kuwa wataendeleza hamasa kwa vijana wa eneo hilo, katika hatua inayolenga kuleta utangamano na uwiano miongoni mwa wakazi wakati huu ambapo siasa zimeanza kushika kasi nchini.
Gamba vilevile ameitaka serikali kuu kutoa mkopo kwa vijana ili waweze kuanzisha biashara ndogo ndogo zitakazo wawezesha kujitegemea maishani.
Katika siku za hivi majuzi, vijana katika eneo la Pwani wamelaumiwa kwa kukubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa kuzua vurugu na kuwahangaisha wenyeji.