Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vijana katika kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani wameombwa kujitenga na makundi ya kihalifu yanayolenga kuzua vurugu pindi uchaguzi mkuu utakapowadia.

Kulingana na afisa wa nyanjani wa Shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ KECOSCE Mwalimu Rama, vijana wanaohusishwa na makundi hayo husababisha maafa na kuziwacha jamii za eneo hilo na majonzi.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kongamano la vijana kwenye ukumbi wa Tononoka, Rama alisema kuwa vijana wanafaa kujihusisha na masuala ya kujiendeleza kimaendeleo na kujitenga na baadhi ya viongozi kama hao ili kudumisha amani eneo hilo.

Aidha, aliwataka vijana kutokubali kuhadaiwa kwa kupewa mlungula ili kuwachagua viongozi hao wakati wa uchaguzi, bali amewataka kuwa waangalifu na kuwachagua viongozi waadilifu.

"Tunawashauri vijana kutokubali kuhadaiwa na baadhi ya viongozi na kuwaunga mkono kuzua vurugu na kusababisha maafa, bali tunawahimiza vijana kuwa waadilifu na kusaidia pakubwa eneo hili kuwa salama," alieleza Rama.

Haya yamejirii baada ya madai kuwa kuna baadhi ya viongozi nchini kuwa wanapanga kuunda makundi maalum ya vijana yatakayozua rabsha kwa wananchi na kuvurugu uchaguzi huo.