Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara ya polisi eneo la Kisauni imewatia mbaroni vijana sita wanaohusishwa na kundi la kihuni la 'Wakali Kwanza'.

Vijana hao wanaaminika kuwa miongoni mwa wale wanaowahangaisha wakazi wa eneo hilo, huku visa vya uhalifu vikiwa vya kiwango cha juu.

Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Ijumaa, mkuu wa polisi eneo la Kisauni Walter Abondo alisema vijana hao watafikishwa mahakamani ili hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Aidha, aliongeza kuwa msako bado unaendelea kuwakamata washukiwa wengine, na wanatumia habari wanayopata kutoka kwa vijana hao waliotiwa mbaroni ili kuendeleza juhudi zao za kuwatia mbaroni.

Mapema wiki jana, kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alitoa onyo kwa wazazi kuwakanya vijana wao kabla ya kuanza msako huo, baada ya visa vya uhalifu kuripotiwa kuongezeka maradufu.