Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa vijana katika Kaunti ya Nakuru wameapa kuwa mstari wa mbele kupigana na ukabila katika kaunti hiyo.

Wakiongoza na rais wa bunge la vijana katika Kaunti ya Nakuru Philip Ngok, vijana hao wamesema kuwa ni jukumu la vijana kusimama kidete na kupigana na ukabila kwa maslahi yao na watu wa Nakuru.

Akiongea katika mkao na wanahabari katika mkahawa wa Stem, Ngok alisema kuwa ukabila umekuwa kikwazo kwa maendeleo katika kaunti ya Nakuru katika miaka iliyopita, na ni wakati wa vijana kumaliza hulka hiyo.

“Sisi kama vijana hatutakaa na kukubali ukabila na siasa za ukabila zitugawanye. Sisi kama viongozi wa vijana tutasimama mstari wa mbele na kuwaongoza vijana wenzetu kuunganisha jamii zote zinazokaa Nakuru,” alisema Ngok.

Ngok aliongeza kuwa kama vijana wataheshimu maoni ya kila kabila katika Kaunti ya Nakuru, na kusema kuwa kila mkenya anayekaa Nakuru ana haki ya kutafuta nafasi ya uongozi.

“Kila mtu hapa awe mluhyia, kikuyu ama msomali na haki ya kugombea kiti na wananchi wakimchagua ni sawa kwa sababu Nakuru si ya kabila flani au flani bali ni yetu sisi sote,” alisema.

Aidha aliwataka vijana kujiepusha kutumiwa na wanasiasa wazee kuzua vurugu na kuendeleza siasa za mgawanyiko haswa msimu huu wa kampeini.

“Kampeini zimefika na hatutaki vijana kutumiwa na watu kuleta shida bali tunataka tuwe kitu kimoja na tuungane kumaliza ukabila,” aliongeza.