Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vijana wa eneo la Pwani wanastahili kusaidiwa katika kuwa wabunifu wa kutafuta ajira kwa kutumia talanta na taalum zao kwa lengo la kuwatenga na maswala ya uhalifu.

Kulingana na afisa mratibu wa mipango wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika Francis Auma Gamba, vijana wamekabiliwa na changamoto ya kiuchumi na wengine kujitosa katika uhalifu kutokana na hali yao kushindwa kujiajiri wenyewe.

Akihutubia kongamano la vijana mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Gamba amesema kwamba sio vijana wote ni wahalifu bali wale wachache ambao wamezama katika masuala ya uhalifu na ugaidi wanapaswa kunasuliwa ili wawe watu muhimu katika jamii.

“Tunawaomba vijana kuwa wabunifu wa ajira na kujisaidia katika kujikimu kimaisha badala ya kutumiwa vibaya na watu fulani na kujiunga na uhalifu kwani hatua ya kubuni ajira itawasadia pakubwa katika kujiendeleza kimaendeleo,” alisema Gamba.

Gamba amewataka maafisa wa polisi kufanya kazi kwa karibu mno na vijana ili kuhakikisha kwamba wahalifu wanatambuliwa na kukabiliwa kikamilifu wala sio vijana kutazamwa kama wahalifu.

Mwanaharakati huyo wa kijamii amedokeza kwamba makongamano ambayo yalifanyika mwaka uliyopita yataendelezwa mwaka huu ili kuwaondoa vijana katika masuala ya uhalifu na ugaidi.