Vijana katika kaunti ya Mombasa wameshauriwa kujiepusha na baadhi ya viongozi wanaolenga kuwatumia vibaya na kuvuruga usalama wa kaunti hiyo ili kujinufaisha kibinafsi.
Akizugumza kwenye kongamano la vijana huko Likoni mjini Mombasa siku ya Jumatano, Afisa wa nyanjani wa Shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ Kecosce Mwalimu Rama amewashauri vijana kuwa katika mstari wa mbele kukataa kutumiwa na kujishughulishwa na masuala muhimu ya kimaendeleo.
Rama amewataka vijana hao kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa polisi katika kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa.
"Tafadhalini vijana kataeni kutumiwa na viongozi wachochezi ili muwaunge katika shughuli zao binafsi na badaye nyinyi ndio mnaangamiza hilo msikubaliene nalo na mjishughulishe na mambo ya kimaendeleo," alisema Rama.
Wakati uo huo Inspekta wa polisi wa Likoni Dafala Ibrahim amewaomba vijana kushirikiana na maafisa wa usalama ili kuboresha usalama.
Kwa upande wao vijana wamefurahishwa na hatua ya Shirika la Kecosce ya kuandaa kongamano hilo na wakasema kuwa litaboresha uhusiano mwema baina ya vijana hao na maafisa wa usalama.