Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana wanaohudumu katika steji ya magari kwenye barabara kuu ya Likoni kuelekea Ukunda wametakiwa kukomesha mwenendo wa kuchukua hatua mikononi na kupiga mtu anayeshukiwa bila kuwa na ushahidi wowote.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mchana katika steji hiyo ya Likoni, mzee wa mtaa wa Likoni Feri Juma Kalu aliwaonya vijana wote dhidi kusingizia wenzao na kuanza kuwapiga.

Juma alistajabishia vitendo na visa ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na vijana hasa manamba wa eneo hilo la kusubiria magari ya kuenda sehemu za Ukunda, Mtongwe pamoja na Kwale, cha hivi karibuni kikiwa cha kijana wa miaka 25 ambaye alipigwa vibaya Jumatatu mchana na kuponea kuchomwa na vijana hao wakishirikiana na baadhi ya wapiti njia.

Kulingana na mzee huyo, ambaye alishuhudia kisa hicho, kijana huyo alishukiwa na mmoja wa muhudumu wa matatu za kwenda Ukunda kuwa alikuwa na nia ya kutaka kumuibia abiria mmoja mizigo yake, kitu ambacho Juma alisema hakikuwa na thibitisho lolote.

“Ilibidi nikaingililia kati na kumuokoa kijana huyo ambaye alikuwa tayari amepigwa mateke pamoja na mawe na vijana hao ambao walikuwa tayari wanakusanyika na hata kuleta tairi ili wapate kumtia moto, hi ni kinyume na sheria,” alisema mzee huyo.