Shirika la kutetea haki za binadamu Huria kwa ushirikiano na taifa la Canada waliandaa siku mbili za tamasha kubwa la burudani mjini Mombasa kwa lengo la kusambaza ujumbe muhimu kwa jamii za eneo hilo.
Tamasha hilo lililopewa jina Youth Theater for Peace Festival lilifanyika siku ya Jumamosi na Jumapili, na lilifunguliwa rasmi na gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pamoja na wawakilishi kutoka nchini Canada.
Miongoni mwa burudani zilizotolewa ni pamoja na nyimbo kutoka kwa wanamziki wa eneo hilo, mashairi na michezo ya kuigiza ambapo ujumbe uliotawala katika sherehe hizo ni amani na vita dhidi ya ukabila.
Tamasha hilo hata hivyo lilitoa nafasi nzuri kwa vijana kujielimisha mambo mengi kuhusu athari za ukabila na vurugu miongoni mwa jamii za Pwani na taifa kwa ujumla.
Akiongea wakati wa tamasha hilo, gavana Joho alishukuru shirika hilo kwa kuandaa kongamano hilo muhimu, na kuwahimiza vijana kutumia vipaji vyao kuelimisha jamii.
“Mombasa imebarikiwa na talanta mbalimbali, na ningewaomba watumie talanta hizo kutangaza vita dhidi ya ukabila, uhasama wa kidini pamoja na kisiasa,” alisema gavana Joho.
Kwa upande wao vijana walioudhuria tamasha hilo walionekana kufurahia burudani pamoja na kujifunza mambo mengi.
“Ukitaka kupitisha ujumbe kwa vijana ni vyema kutumia chombo ambacho wao wanapenda na hapa shirika hili limefikiria zaidi kwa kutumia burudani kuongea na vijana,” alisema Jackson Tsuma kijana aliyeudhuria.
Kati ya wasanii waliotumbiza ni Dazllah pamoja na Susumila ambao ni wanamuziki wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana mkoani Pwani, na hilo pia lilichangia vijana wengi kuhudhuria.