Share news tips with us here at Hivisasa

Kamati ya kuchunguza utumizi wa pesa za serikali katika bunge la kaunti ya Kisii siku ya Jumanne ilirejelea vikao vyake vya kuendelea kuwachunguza mawaziri wa kaunti hiyo jinsi walivyotumia pesa katika wizara zao kwa mwaka wa 2014/15, baada ya kuenda likizo fupi.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, mwenyekiti wa kamati hiyo Ronald Onduso alisema mwaka jana waliwachunguza baadhi ya mawaziri, na kusema watarejelea vikao vyao vya uchunguzi ili kubaini jinsi idara zingine zilitumia pesa za bajeti ili kuwasilisha ripoti kwa bunge la kaunti na kujadiliwa.

Kulingana na Onduso, ni haki kwa mtozwa ushuru kubaini jinsi pesa hutumika katika serikali ya kaunti kuleta maendeleo.

“Siku ya Jumanne tutaendelea na vikao vyetu vya kuwachunguza mawaziri wa idara zile zilizobaki wakati tulienda likizoni ili tuwasilishe ripoti kwa bunge la kaunti,” alisema Onduso.

Hayo yaliafikiwa mwaka jana baada ya kubainika kuwa pesa nyingi hazikutumika kwa uwazi katika wizara mbalimbali, jambo ambalo lilipelekea kila waziri wa idara husika kuchunguzwa kwani ni haki ya wananchi kubaini jinsi pesa zao zinatumika kuleta maendeleo.

Aidha, Onduso alisema kamati yake itajaribu kila iwezalo kuhakikisha pesa za wananchi zinatumika vizuri na kwa njia ya uwazi kuleta maendeleo katika sehemu mbalimbali za Kaunti ya Kisii.