Gavana wa kaunti ya Nakuru imeonyesha masikitiko yake kwa kuwa na idadi kubwa ya baa ikilinganishwa na shule za msingi na za upili kwa ujumla.
Akizungumza alipozindua kamati za kusimamia utoaji wa leseni, kudhibiti uuzaji, usambazaji na utayarishji wa vileo katika kaunti ya Nakuru mwishoni mwa juma lililopita, gavana Kinuthia Mbugua alisema kuna jumla ya baa elfu moja mia tisa na hamsini huku kukiwa na shule elfu moja mia sita na sabini na tano.
Huku kamati hizo ambazo zimesambazwa katika maeneo bunge kumi na moja, Mbugua alisema kuwa zinawajibu wa kuhakikisha zinazingatia kanuni zilizowekwa kupitia sheria iliyopitishwa katika bunge la kaunti ya Nakuru na kutiwa sahihi na kuwa sheria ya mwaka 2014 inayodhibiti vileo.
Hata hivyo, mkuu wa kaunti hiyo alisema kuwa eneo bunge la Nakuru Mashariki ndilo linaloongoza na baa zaidi ya mia nne huku eneo bunge la Kuresoi Kusini likiwa na idadi ndogo ya baa arobaini.
Kadhalika aliongeza kuwa kuna viwanda 11 ambavyo vimeruhusiwa kutengeneza vileo katika kaunti hiyo.
Hata hivyo Gavana huyo alisema kuwa kamati hizo zitaanza kutekeleza wajibu wao kuanzia Januari 15 mwakani.