Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa mrengo wa Cord wamekita kambi Malindi kuwarai wakaazi wa eneo hilo kumchagua mgombea wa kiti cha ubunge kwa tikiti ya ODM Willy Mtengo.

Wakiongozwa na Kinara wa mrengo huo Raila Odinga, viongozi hao wamesema kuwa wakati umefika sasa wa kufanya mabadiliko na kumchagua kiongozi mwaadilifu na kujiepusha na viongozi wafisadi na wanyanyasaji katika jamii.

Raila aliwataka wakaazi wa eneo bunge hilo kuhakikisha kuwa wanafanya uamuzi wa busara kwenye uchaguzi huo mdogo wa Malindi wa tarehe 7 mwezi Machi, huku akiwataka kujiepusha na watu walaghai wasiopenda demokrasia nchini.

“Nataka kuwahimiza wakaazi wa Malindi muwe makini na viongozi walaghai na wanyanyasaji kwani wengi wao hupenda kujibinafsisha wenyewe. Ni lazima wakaazi wa eneo hili kufanya maamuzi bora,” alisema Raila.

Kwa upande wake, kinara mwenza wa mrengo huo Kalonzo Musyoka, aliwashinikiza wakaazi kumchagua Willy Mtengo ili kuwatekelezea miradi ya maendeleo na kuwarai kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli hiyo ya upigaji kura.

“Tafadhali wakaazi jitokezeni kwa wingi kwenye shughuli ya upigaji kura siku ya Jumatatu na kumchagua Willy Mtengo ili tufanye kazi pamoja na tuhakikishe kuwa demkrasia inatekelezwa vyema, na kuwaondoa madarakani viongozi wafisadi,” alisema Kalonzo.

Shughuli hiyo ya upigaji kura itafanyika siku ya Jumatatu huku Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ikijiandaa katika shughuli hiyo.