Baadhi ya viongozi wa mrengo wa Cord wamekashifu hatua ya baadhi ya viongozi wenza kutoka Pwani kujiunga na chama kipya cha Jubilee, wakisema kuwa viongozi hao wamefanya hivyo kwa maslahi yao ya kibinafsi.
Viongozi hao walidai kwamba serikali ya Jubilee imeshindwa kutatua tatizo sugu la umiliki wa ardhi Pwani, pamoja na ongezeko la vijana kuuwawa kwa kupigwa risasi kiholela kwa kisingizio cha kukabili ugaidi nchini.
Wakizungumza kwenye hafla tofauti siku ya Jumanne, katika Kaunti ya Mombasa, Mbunge wa Msambweni Suleiman Dor na mbunge mteule Zulekha Hassan, walipuzilia mbali ziara ya kimaendeleo ya Raisi Uhuru Kenyatta katika eneo la Pwani.
Wawili hao walidai kuwa ziara hiyo inalenga kuwashawishi wakaazi wa Pwani kujiunga na Jubilee bali sio ziara ya maendeleo kama inavyodaiwa.
Zulekha ameipuzilia mbali hatua ya rais ya kuwapa hati miliki za ardhi wakaazi katika Shamba la Waitiki, akiitaja hatua hiyo kama njama ya kisiasa ili kuwashawishi waunge mkono serikali ya Jubilee.
Zulekha na Dori aidha wamekejeli hatua ya baadhi ya wabunge wa Pwani wakiwemo mbunge wa Lungalunga Khatibu Mwashetani, Zainabu Chidzuga wa Kwale, Masoud Mwahima wa Likoni, Gideon Mung’aro miongoni mwa wengine waliojiunga na Jubilee kama wanaolenga kujinufaisha kibinafsi.