Viongozi wa dini mbalimbali wamehimizwa kujitokeza katika mikutano ya kueneza jumbe za amani kama njia mojawapo ya kumkaribisha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Naibu Askofu wa Jimbo kuu la Mombasa Padri Wilbard Lagho alisema kwamba maombi hayo ndiyo yatakayoleta uhusiano mwema baina ya tabaka mbalimbali katika Kaunti ya Mombasa, na kuleta mwamko mpya kwa wakazi na waumini wa dini mbalimbali katika kaunti hiyo.
Padri Lagho alisema kushuhudiwa msukosuko wa kiusalama katika Kaunti ya Mombasa na eneo zima la pwani, kumeleta mtizamo mbaya kwa mataifa ya magharibi na iwapo wapwani wataungana na kueza amani kwa kutumia fursa ya ziara ya Papa Francis basi eneo hilo litakuwa salama.
"Tunawahimiza viongozi wa kisiasa, dini, tamaduni na jamii kujitokeza na kuungana na wenzao katika mkutano wa amani tutakaoundaa ili kueneza ujumbe wa amani. Nadhani hatua hii itasaidia pakubwa kupunguza visa vya uhalifu na malumbano ya kila uchao,” alisema Padri Lagho.
Tayari waumini wa dini ya Kikristo ya Katoliki mjini Mombasa wanakamilisha maandalizi yao ya kuelekea jijini Nairobi kwa ibada maalum itayoongozwa na Baba Mtakatifu Papa Francis katika ziara yake ya siku tatu humu nchini.