Share news tips with us here at Hivisasa

Wito umetolewa kwa viongozi wa kidini katika eneo la Pwani kuwashauri vijana na akina mama kushiriki katika zoezi la usajili wa wapiga kura ili kuwawezesha kushiriki moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake nchini Sureya Hersi, zoezi hilo huenda likaathirika kutokana na jamii kukosa ufahamu nahasa kuhusiana na zoezi hilo.

Hersi alipendekeza shughuli hiyo ya hamasa kufanywa hadi katika maeneo ya mashinani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatato, Hersi alisema kuwa iwapo viongozi hao watajitokeza katika kuwashinikiza vijana na akina mama kujisajili katika zoezi hilo, basi idadi kubwa ya wakaazi watajitokeza kisajiliwa.

“Tunawaomba viongozi wa kidini kujitokeza na kuwahamasisha vijana na akina mama mashinani kufahamu umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura, ili waweze kuchagia pakubwa katika maswala ya demokrasia na uongozi nchini,” alisema Sureya.

Kiongozi huyo wa wanawake nchini ameahidi kuzuru mashinani na kuwahamasisha wanawake na vijana kujitokeza kwa wingi katika kipindi cha zoezi la usajili wa wapiga kura ili kuhakikisha kuwa wanawake zaidi wanachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao.