Viongozi wa kidini mjini Nakuru wamepinga vikali madai ya baadhi ya wanasiasa kuwa ukahaba uhalalishwe.
Akiongea kwenye kanisa la St Geralds Nakuru siku ya Jumapili, kasisi Peter Maina alisema viongozi wa kisiasa wanafaa kutafuta suluhu la mauaji yanayoendelea mjini Nakuru dhidi ya makahaba wala si kusema watafanyia sheria marekebisho kuruhusu biashara hiyo.
"Nimeshangaa sana eti baadhi ya wabunge hapa kwetu Nakuru wamesema turuhusu ukahaba ili kuzuia mauaji. Mbona wasiseme tumalize ukahaba kabisa na hilo ndio suluhu la kudumu?" alisema kasisi Maina.
Maina alikuwa akikosoa mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria aliyenukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema atapeleka mswada bungeni ili kuruhusu ukahaba.
Kasisi Maina alisema ukahaba ni kinyume cha itikadi za kiafrika na pia dini.