Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi wa kidini wameunga mkono hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri, kama hatua mojawapo ya kukabiliana na ufisadi.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Katibu mtendaji wa Baraza la Maimam na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, alisema kwamba hatua aliyoichukua Rais Kenyatta inaonyesha wazi kuwa amejitokeza kutumia mamlaka yake kikatiba kuangamiza ufisadi nchini.

Kulingana na Shiekh Khalifa iwapo rais atachukua jukumu la kupigana na maafisa wafisadi kikamilifu, basi taifa hili litaimarika kiuchumi na uangamiza umaskini.

Alimshinikiza Rais Kenyatta pamoja na Naibu wake William Ruto kutorudi nyuma katika vita dhidi ya ufisadi nchini.

"Tunampongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuteuwa baraza jipya la mawaziri. Hatua hiyo imeidhirisha kuwa amejitokeza kupigana vilivyo na ufisadi nchini. Hatua aliyochukua yeye na Naibu wake William Ruto itainua uchumi wa nchi na kuangamiza umaskini. Sisi tuko pamoja naye katika vita dhidi ya ufisadi,” alisema Sheikh Khalifa.

Kiongozi huyo wa kidini amemtaka Rais Kenyatta pamoja na Naibu wake William Ruto kuliokoa taifa kutokana na janga la ufisadi, iwapo wanawataka Wakenya kuwapigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.