Viongozi wa kanisa kutoka kaunti ya Nakuru chini ya mwavuli wa Likia Beyond Peace and Conflict Resolutuion, wamewataka viongozi wa kidini kote nchini kuisaidia serikali katika kueneza habari kuhusu umuhimu wa wananchi kujisajili kuwa wapiga kura.
Akiwahutubia wanahabari mjini Nakuru Jumatano viongozi hao wakiongozwa na askofu Abraham Gitu wamesema kuwa kanisa lina uwezo na jukumu la kuhamasisha wananchi kutokana na imani ya waumini wao.
Akilitaja kanisa kama mwangaza wa taifa, Gitu amesema kuwa ili serikali kuafikia malengo yake kikamilifu, ipo haja viongozi hao wa makanisa kushirikiana na serikali iliyoko mamlakani na wala sio kupingana nayo akitaja kuwepo kwa vuta ni kuvute kama chanzo cha kusalia nyuma kimaendeleo.
“Kanisa ni kurunzi ya taifa maanake linatoa mwelekeo na maadili yanayokubalika na jamii na taifa kwa jumla,” Gitu alisema.
Kuhusu kipindi cha mwezi mmoja ambacho serikali imetenga kwa zoezi hilo la usajili chini ya tume ya IEBC, Gitu amesema kuwa ni muda unaotosha iwapo zoezi hilo litafanyika kwa mpangilio na utaratibu.
“Muda wa mwezi mmoja ambao serikali katika zoezi zima la usajili wa wapiga kura unatosha kabisa ikiwa kutakuwa na mpangilio,” alisema.