Viongozi wa kidini katika eneo la Olposimoru kwenye kaunti ya Narok wamehimizwa kujitokeza na kutoa mwelekeo ufaao kwa jamii zinazozozana kwenye eneo hilo.
Himizo hilo limetolewa na Askofu Abraham Gitu wa baraza la Likia and Beyond Peace and Conflict Resolution aliyezungumza na wanahabari Jumatatu ya leo ya tarehe 28 Desemba baada ya kuzuru eneo hilo wikendi iliyopita .
Kulingana naye, wengi wanawaamini na wana imani na viongozi hao wa kidini, na kutokana na hilo, wana wajibu wa kuleta pamoja jamii hizo zinazozozana.
Kando na hilo, amesisitiza kwamba itakuwa hatia kwa viongozi wa kidini kuketi kitako na kushuhudia watu wakiwashambuliwa na wenzao, huku wengine wakiteketeza nyumba za wenzao.
Kulingana naye, maafisa wanaodumisha usalama hawawezi kufanikiwa peke yao katika kurejesha Amani katika eneo hilo la Olposimoru bila kuungwa mkono na viongozi wa eneo hilo.
Mapigano hayo yalianza baada ya wafugaji wawili kuuwawa kwa mishale walipokuwa wakilisha mifugo wao.
Wabunge kadhaa na wawakilishi wa wadi tayari wamekashifu ghasia hizo .