Viongozi wa makanisa wamehimizwa kuwajibikia matumizi ya pesa zinazotengewa miradi mbalimbali ya kanisa.
Akiwahutubia waumini wa Kanisa la PAG kule matutu siku ya Jumapili, mhubiri Ronald Ogetonto, alisema kuwa uongozi wa kanisa unaendelea kuathiriwa kutokana na matumizi mabaya ya pesa za kanisa.
"Uongozi wa makanisa mbalimbali unaendelea kuathirika pakubwa kutokana na matumizi mabaya ya pesa zinazo stahili kufadhili miradi muhimu ya kanisa. Inastahili tufanye kazi kwa uwazi ili watu wengine waige mfano kutoka kwetu," alisema Ogetonto.
Ogetonto aidha aliongeza kwa kusema kuwa ni jambo la aibu kwa baadhi ya viongozi wa makanisa kujihusisha na visa vya ufisadi ilhali wao ndio wanaostahili kuwa katika mstari wa mbele kupiga vita ufisadi.
"Ni jambo la aibu kusikia kuwa baadhi ya viongozi wa makanisa ndio wanaojihusisha pakubwa na visa vya ufisadi. Kwa kweli hilo halifai kwa kuwa yatupasa kufahamu kuwa sisi ndio kioo cha jamii," alisema Ogetonto.