Hisia mbali mbali zimetolewa na wakazi wa Kisumu kuhusu ahadi zilizotolewa na viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita kuwawakilisha,
Wakazi hao walisema kuwa kufikia sasa bado viongozi hao hawajatimiza ahadi hizo ilhali uchaguzi mwingine mkuu unakaribia.
Katika mahojiano na baadhi ya wakaazi siku ya Jumatano, wengi wao walielezea kutamaushwa kwao na hatua ya viongozi waliowachagua wakiwemo wawakilishi wadi, wabunge, maseneta na hata magavana, kukosa kushugulikia mahitaji yao ya kimsingi kama walivyoahidi wakati wa kampeni zao mwaka 2013.
''Viongozi wa siku hizi wanajihusisha na siasa tupu na matusi pekee. Hakuna maendeleo wanayowaletea wakazi,” alisema mmoja wa wakaazi aliyejitambulisha kama Tom.
Wakazi hao walisema kuwa maswala muhimu ya miundo msingi kama vile barabara, hospitali miongoni mwa mahitaji mengine yamesalia kuwa changamoto kwao, huku baadhi ya viongozi wakipuuza lalama za wananchi.
Baadhi yao walitaja kutoelewa vizuri katiba ya nchi na majukumu ya afisi mbali mbali za serikali za ugatuzi, hasaa kuhusiana na jukumu la kila mmoja kama mojawapo ya sababu inayopelekea wengi wa viongozi wa kisiasa kuwa na nafasi ya kujitetea na kuwadanganya wananchi hata zaidi.
Vile vile wakazi hao walikosoa Rais Uhuru Kenyatta na utawala wake kwa ujumla kwa kukosa kutimiza baadhi ya ahadi alizotoa.