Viongozi wa mtaa wametakiwa kusaidia katika kupunguza visa vya utovu wa usalama kwenye mitaa wanakoishi na kuhakikisha kuwa jamii wanayoiongoza inawajibika ipasavyo.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu, naibu wa afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Likoni Anthony Shimoli alisema kuwa jamii kwa kushirikiana na viongozi waliopewa jukumu la kusimamia usalama mitaani, wataweza kuepusha visa vya mashambulizi kutoka kwa magenge ya uhalifu.
Shimoli alisema kuwa idara yao imeweka mikakati maalumu kuona kuwa usalama unaimarishwa katika eneo hilo.
Alisema kuwa visa ambavyo vilikuwa vinashuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya wilaya hiyo ambapo magenge ya vijana yalikuwa yanawahangaisha wakazi vimepungua.
Wakazi ambao walizungumza na mwandishi huyu walishukuru idara hiyo kwa kuweka juhudi za kuona kuwa visa vya uhalifu vimepungua.
Walisema kuwa wapo tayari kutoa ripoti katika vituo vya usalama husika na kuwataka jamii na wakazi wanaoishi maeneo hayo kwa jumla kushikana mikono kufanikisha mpango huo.
“Kuna nafuu kwenye usalama hasa nyakati za usiku, ambapo watu walikuwa wakishambuliwa. Sasa polisi wanashika doria na tunawapongeza japokuwa kuna visa vichache miongoni mwa wahuni. Tunaamini kuwa idara husika itaendelea kukaza misuli katika kutokomeza uhalifu kabisa,” alisema mkazi mmoja wa Likoni.
Eneo hilo la Likoni ni miongoni mwa maeneo mengi katika Kaunti ya Mombasa ambayo yamekuwa na visa kadhaa katika siku za hivi karibuni, za kuvamiwa na makundi ya vijana kama Wakali Kwanza.
Idara za usalama sasa zimesema kuwa zinachukua hatua imara ili kupunguza visa hivyo.