Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa katika eneo la Pwani wamehimizwa kutathmini idadi ya vijana katika eneo hili ili kuwawezesha kutenga kiasi cha fedha zitakazoweza kukimu vijana ndoto zao katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.

Akiongea kwenye kongamano la vijana la kimaendeleo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Afisa wa nyanjani katika shirika la kijamii la ‘Kenya Community Suppport Centre’ Kecosce, Mwalimu Rama amesema kuwa hatua hiyo itasaidia viongozi kutekeleza miradi ya kimaendeleo mashinani.

Rama amesema kuwa kutokana na ukosefu wa ufahamu wa viongozi idadi kamili ya vijana katika eneo hili pamoja na kutofahamu wanachohitaji vijana kutekelezwa na viongozi kumechangia pakubwa vijana kushindwa kujikimu kimaisha.

"Tunawataka viongozi kutathmini idadi ya vijana katika eneo la Pwani na kuhakikisha kuwa fedha wanazohitaji kuwafanyia vijana maendeleo zinatosha ili kuwawezesha vijana kujikimu kimaisha," alisema Rama.

Wakati uo huo amewahimiza vijana kujitolea kikamilifu na kujisajili kama wapiga kura ili kubadilisha uongozi wa taifa hili kwa kuwachagua viongozi waadilifu.

Mwanaharakati huyo ameahidi kuzuru mashinani na kuwapa hamasa vijana na jamii ili kufahamu masuala muhimu ya kimaendeleo.