Viongozi wa kisiasa na wale wa kidini katika kaunti ya Nakuru wamehimizwa kudumisha na kukumbatia amani hasua wakati huu ambapo tunaelekea mwaka mpya wa 2016.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Nakuru jumanne, mwakilishi mteule wa wadi katika kaunti ya Nakuru Catherine Njeri Waweru na askofu wa dhehebu la Kenye Assembly Messiah Israel Church, Abraham Gitu, walikariri kuwa mwaka wa 2015 ulikuwa na changamoto si haba kama vile ajali za barabarani, visa vya ugaidi na vifo vilivyotokana na unywaji wa pombe haramu.
Huku akitaka wakristu wakabidhi taifa hili mbele ya mungu na pia kuombea amani, askofu Gitu alisisitiza kwamba mzozo uliotokea katika eneo la Olposomoru wikendi iliyopita unafaa kushtumiwa vikali na pia unafaa kutumika na jamii zingine kutambua kwamba vurugu sio suluhu la mizozo.
Askofu Isaac Kariuki wa dhehebu la Full Gospel Churches of Kenya aliwahimiza viongozi wa kidini kuiombea Kenya ili iweze kuwa na amani.
Alirejelea tukio la tarehe desemba 20 mwaka huu la Mandera ambapo waislamu waliwakinga wenzao wakristu dhidi ya kuuwawa na magaidi wanaokisiwa kuwa wa kundi la al Shabaab.
"Ningewahimiza viongozi wote wa kidini kuiombea Kenya hasua tunapoelekea mwaka mpya ili tuweza kuwa na amani. Pia nawashukuru waislamu kwa kuwakinga wakristu huko Mandera ambapo karibu wauwae na magaidi wanaoshukiwa kuwa wa kundi la al Shabaab. Hilo ni jambo ambalo lilidhihirisha upendo mkubwa katika ya ndugu,’ alisema askofu Kariuki.
Wakati huo huo, askofu Kariuki aliishukuru serikali kwa kuchukua hatua za kukabiliana na ghasia katika eneo la Olposimoru, kaunti ya Narok pamoja na kukabiliana na pombe haramu.
"Tunawahimiza wenzetu walio katika mpaka wa kaunti za Narok na Nakuru kudumisha amani. Tunataka amani iwe hapa Kenya. Tunamuomba mwenyezi Mungu arejeshe hali ilivyokuwa katika eneo hilo," aliongeza askofu Kariuki.
Kando na hayo, bi Njeri aliwahimiza vijana kujiepusha na unywaji wa pombe haramu pamoja na tabia ambazo huenda zikawadhuru katika siku za hapo baadaye.
"Nawasihi wakenya wote katika mwaka ujao wa 2016 tufanye kazi na pia tujiepushe na madawa ya kulevya na pombe haramu haswaa kwa vijana wetu. Tuweze kujenga nchi yetu ili iweze kupata heshima inayostahili," aliongeza mwakilishi huyo mteule wa wadi.