Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kituo cha kupambana na utumizi wa dawa za kulevya eneo la Pwani cha 'Reach out Centre Trust' kimewashinikiza viongozi wa kisiasa na maafisa wa polisi kuwashauri vijana waliyoathirika na utumizi wa mihadrati kupata tiba maalum.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho, Taib Abdulrahman, kuna zaidi ya maeneo 100 yaliyoorodhesha kuwa na asilimia kubwa ya vijana waliyoathirika na utumizi wa dawa za kulevya hasa katika eneo la Pwani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Abdilrahman alisema kwamba maeneo ya Marikani, Jomvu na Kisauni yana idadi kubwa ya vijana wanaotumia dawa za kujidunga sindano huku maeneo ya Malindi na Ukunda yakiorodhesha idadi kubwa ya watumizi wa heroine.

Abdulrahman alisisitiza umuhimu wa serikali na mashirika ya kijamii kujitokeza na kuwahamasisha vijana mashinani kuhusu jinsi ya kujiepusha na utumizi wa dawa za kulevya kwa kuwa dawa hizo huathiri hali yao ya kiafya.

“Tunawaomba viongozi na maafisa wa polisi kuwajibikia makujumu yao vyema kwa kuwashauri vijana waliyoathirika na utumizi wa mihadarati kujiwasilisha kwa mashirika ya kupambana na utumizi wa mihadarati ili wapate ushuri nasaa na matibabu,” alisema Abdulrahman.

Wakati huo huo, ameitaka serikali kuwachunguza walanguzi wakuu wa mihadarati eneo la Pwani na kuwachukulia hatua kali za kisheria ili kusitisha kuenea kwa dawa hizo za kulevya.